MWANI KUINGIZWA WRS KUIMARISHA MNYORORO WA THAMANI- MHE.LONDO
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, ameliambia Bunge kuwa Serikali, kupitia Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), imeanza mchakato wa kuliingiza zao la mwani katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS) ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao hilo na kumlinda mzalishaji.
Mhe. Londo ameyasema hayo Bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Asha Omar Rashid, aliyehoji kuhusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wakulima wa zao la mwani wanapata bei yenye tija.
Akijibu swali hilo, Mhe. Londo amesema Serikali imeweka mkakati mahsusi wa kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mwani, ikiwemo kufanya tafiti kuhusu upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa zao hilo.
Amesema kupitia WRRB, Serikali imeanza kuangalia utaratibu wa kuliingiza zao hilo katika Mfumo huo ili kulinda bei na wazalishaji.
