WADAU RUKWA WAKUBALIANA MAHINDI KUUZWA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA
WADAU RUKWA WAKUBALIANA MAHINDI KUUZWA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA
WADAU wa zao la mahindi mkoani Rukwa wamekubaliana kuuza mahindi kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na mnada wa kwanza unatarajiwa kufanyika mwezi Agosti, 2026, ili kuimarisha biashara ya zao hilo, kuongeza uwazi wa soko na kuwawezesha wakulima kupata bei zenye ushindani.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao cha wadau kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, Julai 28, 2026, kilicholenga kujadili maandalizi ya kuanza kutekeleza mfumo huo kwenye zao la mahindi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wawakilishi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Wakuu wa Wilaya za Nkasi na Kalambo, viongozi wa vyama vya ushirika, Umoja wa Wafanyabiashara pamoja na wakulima.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Makongoro amewataka wadau wote kushirikiana kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kwa ufanisi ili kuongeza tija kwa wakulima na kuimarisha masoko ya mahindi mkoani humo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mauzo ya mahindi yatafanyika kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kutumia Meneja Dhamana, huku minada ikiratibiwa kupitia vyama vya ushirika.
