WATENDAJI WA GHALA WAIPONGEZA WRRB, WAAHIDI KUWA MABALOZI WA WRS
Washiriki wa mafunzo ya watendaji wa ghala kuelekea msimu wa korosho 2026/27 wameipongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa kuandaa mafunzo hayo, wakisema yamewaongezea uelewa kuhusu matumizi na manufaa ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS) katika biashara ya mazao.
Wakizungumza leo, Septemba 16, 2026, baada ya kupatiwa mada kuhusu mfumo huo, washiriki hao wamesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutambua na kuhakiki ubora wa bidhaa zinazoingizwa ghalani ili kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyohitajika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hususan katika usimamizi wa ubora wa korosho kuelekea msimu wa biashara wa 2026/27.
Washiriki hao wameahidi kuwa mabalozi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kuwaelimisha wakulima na wamiliki wa maghala kuhusu manufaa ya mfumo huo, ikiwemo kuimarisha uwazi katika biashara, kuongeza ushindani wa bei na kuwezesha wakulima pamoja na wanunuzi kunufaika na biashara ya mazao.
