WRRB YAWANOA WATENDAJI WA GHALA KUELEKEA MSIMU WA KOROSHO 2026/27
BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeanza kuwapatia mafunzo watendaji wa ghala zaidi ya 100 kwa ajili ya msimu wa korosho wa 2026/27, huku ikiahidi kuimarisha usimamizi wa ubora wa zao hilo ili kukidhi viwango vya soko la ndani na kimataifa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa watendaji wa ghala mkoani Mtwara leo Septemba 14, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu Huduma wa WRRB, Mwita Thomas, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo na kuongeza uelewa wa namna ya kusimamia ghala na kuhakikisha korosho zinazopokelewa na kuhifadhiwa zinakidhi viwango vya ubora kwa mujibu wa miongozo iliyopo.
“Mafunzo haya yatakuwa chachu kwa washiriki katika kuongeza tija na kuimarisha usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika zao la korosho,” amesema Bw. Thomas.
Amesema usimamizi madhubuti wa maghala ni muhimu katika kulinda ubora wa korosho na kuongeza ushindani wa zao hilo katika soko, hatua inayotarajiwa kuongeza manufaa kwa wadau wa mnyororo wa thamani.
Aidha, amewahakikishia wanunuzi watakaoshinda katika minada ya korosho kuwa WRRB itaendelea kusimamia ubora wa zao hilo kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa ili kuhakikisha wanapata bidhaa yenye ubora unaolingana na taarifa zilizotolewa wakati wa biashara.
