Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
AMCOS zote kufungiwa mizani ya kieletroniki
20 Jul, 2022
AMCOS zote kufungiwa mizani ya kieletroniki

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghala nchini Bw.Asangye Bangu amesema wanatarajia kuimarisha matumizi ya mizani ya kieletroniki katika vyama vyote vya msingi ili kupunguza changamoto ya tofauti ya malipo ambayo imekuwa inalalamikiwa na wakulima wakati wa malipo.

Amesema mizani ya kieletroniki inaonesha namba bila utata kwa wakulima na kwamba mizani hiyo imeanza kugawiwa katika mikoa inayonunua mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwemo Mkoa wa Kagera ambao tayari umepelekewa mashine zaidi ya 180.

"Uzuri wa mashine za kieletroniki ikisoma uzito unaingia moja kwa moja kwenye kazi data na kutoa karatasi yenye data zote badala ya kuandikwa kwa mkono",alisema Bangu.

Akizungumza na wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika Nanyumbu mkoani Mtwara amesema Ofisi yake pia inaimarisha matumizi ya TEHAMA kwenye mfumo huo ili kuondoa kero kwa wakulima kwenye mfumo wa malipo.

Amesema katika ziara yake ya kutembelea wakulima kwenye vyama vya Msingi amepata malalamiko kuhusiana na changamoto chache zinazotokea kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.

Hata hivyo amesema wakulima wanaukubali mfumo huo hivyo wameshauri changamoto hizo zipatiwe ufumbuzi ili mfumo huo uwe na tija kubwa kwa wakulima.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu  Baraka Mlangwa amesema wakulima wanafaidika kutokana kutumika mfumo wa stakabadhi ghalani hasa katika mazao ya ufuta na korosho .

Amesema wananchi wanauza mazao yao kwa bei nzuri na kuna Usalama wa kutosha wa fedha zao kwa sababu malipo yanapitia benki.

Kwa upande wake Afisa Ushirika wa  Wilaya ya Nanyumbu Daniel Mlungu ameyataja makusanyo ya ufuta msimu huu kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa yamefikia zaidi ya tani 2200 na kwamba kilo moja ya ufuta imefikia shilingi 3000.

Baadhi ya wakulima wa AMCOS ya Nanyumbu wamepongeza mfumo huo kutumika kwa wakulima ambao wameutaja kuwa na faida nyingi ukilinganisha na hasara.

Mzee Hamisi Lilangunda amesema Mfumo wa Stakabadhi za ghala umewaokoa kutoka mfumo wa uuzaji mazao holela ambao ulokuwa una mnyonya mkulima kwa miaka mingi.

Said Mpopera ameomba changamoto za kuchelewa kwa malipo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani zitafutiwe ufumbuzi sanjari na kuchelewa kwa pembejeo za kilimo katika zao la korosho kuna punguza uzalishaji wa zao hilo ambalo linategemewa na wakulima wengi.

Mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara ndiyo mikoa inayoongoza kwa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za ghala hali iliyosababisha wakulima kupata tija kwenye kilimo