MIFUGO KUINGIA KATIKA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA

*MIFUGO KUINGIA KATIKA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA*
Dodoma, 18 Agosti 2025 – Hatua mpya ya mageuzi katika sekta ya mifugo imechukua sura mpya baada ya Bodi ya Stakabadhi za Ghala (WRRB) kushirikiana na Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kujadili nafasi ya mifugo kwenye mfumo wa stakabadhi za ghala.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, alieleza kuwa mifugo inapohifadhiwa katika maeneo maalumu huweza kutambulika kama ghala, jambo litakalosaidia kuimarisha biashara ya mifugo nchini. Aliongeza kuwa kuwepo kwa bima ya mifugo kutalinda wafugaji dhidi ya magonjwa, wizi na vifo vya mifugo, huku akisisitiza kuwa unenepeshaji ni nyenzo muhimu ya kuongeza thamani kabla ya mifugo kuingia sokoni kupitia mfumo wa stakabadhi.
Kwa upande wake, CCWT ilibainisha changamoto kubwa zinazowakabili wafugaji, ikiwemo kutoshirikishwa ipasavyo kwenye mfumo, uhaba wa malisho na ranchi, pamoja na sheria zinazowaathiri moja kwa moja. Hata hivyo, wadau wote waliungana katika hoja ya kwamba elimu kwa wafugaji na kuboresha masoko ya mifugo ni mambo ya msingi ili mfumo huu uweze kufanikiwa.
Katika maazimio ya kikao hicho, pande zote zilikubaliana:
1. Kuunda kikosi kazi maalum kitakachoratibu na kuendesha majaribio ya mfumo.
2. Viongozi wa kanda kuainisha maeneo mahsusi ya wafugaji yatakayotumika kama vituo vya majaribio.
3. Kuanza na ranchi za serikali, mashamba binafsi na maeneo yenye mpango bora wa matumizi ya ardhi.
4. Kusajili wafanyabiashara wa ng’ombe na kuwaingiza rasmi kwenye mfumo wa stakabadhi.
Mwisho wa kikao uliashiria dira mpya: mfumo wa stakabadhi za ghala unaweza kubadilisha kabisa ufugaji wa Tanzania kutoka wa kujikimu na kuwa wa kibiashara, endapo changamoto zilizopo zitashughulikiwa kwa pamoja.