Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA WAWANUFAISHA WAKULIMA
14 Jul, 2022
MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA WAWANUFAISHA WAKULIMA

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imesema idadi kubwa ya wakulima wa mazao mbalimbali nchini wamepata mafanikio makubwa na kunufaika na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Hayo yamesemwa na Afisa Udhibiti Ubora wa Bodi hiyo Bi. Witness Temba kwenye Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Mfumo huu umesaidia wakulima kupata taarifa na takwimu mbalimbali za mazao kwa wakati na usahihi, awali kabla ya uwepo wa mfumo huu ilikuwa ni ngumu kupata taarifa pamoja na takwimu mbalimbali za mazao kwa wakati na usahihi ilikua inachuka hata wiki kupata taarifa na takwimu hizo na saa nyingine zinakuwa sio sahihi, lakini baada ya uwepo mfumo huu imekuwa rahisi kupata takwimu na taarifa zote muhimu za mazao hayo.

Aidha, uwepo wa mfumo huu umechangia katika kuongeza uzalishaji wa mazao kwa mwaka kwani mkulima anapata fursa ya kuuza mazao yake kwa bei ya faida hivyo, huchochea wakulima kuongeza kwa wingi ulimaji wa mazao yenye tija na ubora zaidi na kuongeza thamani ya mazao hayo.

“Mfano zao la Kakao kule Kyera, Mkoani Mbeya na Mvomero, Mkoani Morogoro kuna tofauti kubwa ya mauzo ya mazao hayo kabla ya mfumo na baada ya mfumo, bei zimekuwa na tija na ongezeko ambalo ni kubwa sana kwa Wakulima”, amesema Bi. Temba.

Vilevile, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umesaidia kukuza huduma za kifedha vijijini kwani wakulima huwasilisha mazao yao katika vyama vya Ushirika, malipo na manunuzi yote ya mazao hayo hufanyika kupitia taasisi za kifedha(Benki) hivyo hupelekea kukuza huduma za kifedha katika eneo husika.

Kadhalika Serikali inapata mapato yake katika uuzaji wa mazao kupitia mfumo huu, awali kabala ya uwepo wa mfumo huu uuzaji wa mazao ulikua unafanyika kiholela na kupelekea kuikosesha Serikali mapato yake, kwa uwepo wa mfumo huu kumesaidia Serikali kupata mapato yake kuanzia kwenye uuzaji hadi usafirishaji wa mazao hayo nje ya nchi.

Bi. Temba ameendelea kueleza kuwa utaratibu wa mnada wa mazao unakuwa na ushindani zaidi na kupelekea uvumbuzi wa bei zenye tija kwa wakulima, mfano zao la Korosho bei yake inamarika msimu hadi msimu na hii ni kutokana na matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imepewa Mamlaka ya kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mfumo wa Stakabadhi za Ghala na imeanzishwa lengo la Urasimishaji wa Biashara, hususani kwenye mazao ya Kilimo na ipo chini ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.