Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
WAZIRI KAPINGA ATOA MWELEKEO MKAKATI KUWAWEZESHA WAKULIMA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA
26 Feb, 2026
WAZIRI KAPINGA ATOA MWELEKEO MKAKATI KUWAWEZESHA WAKULIMA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA

WAZIRI KAPINGA ATOA MWELEKEO MKAKATI KUWAWEZESHA WAKULIMA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga (Mb), amezitaka Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kuandaa na kutekeleza mkakati jumuishi wa kuwawezesha wakulima kuanzia hatua za uzalishaji, ukusanyaji, uhifadhi hadi uuzaji wa mazao, ili kuongeza tija na kuhakikisha wakulima wananufaika na bei nzuri sokoni.

Kauli hiyo imetolewa Leo Februari 25, 2026 wakati wa hafla ya kufunga msimu wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa msimu wa 2025/2026 na kufungua rasmi msimu mpya wa 2026/2027, iliyofanyika katika Mkoa wa Simiyu. Waziri Kapinga amesema kuwa mafanikio ya mfumo huo yanategemea kwa kiasi kikubwa elimu kwa wakulima na wadau, pamoja na uwepo wa miundombinu bora ya maghala na usimamizi madhubuti wa masoko.

Aidha, Waziri ameiagiza WRRB kuimarisha utoaji wa elimu na uhamasishaji kwa wakulima, wafanyabiashara, wasimamizi wa maghala na wadau wengine muhimu, ili kuongeza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wamiliki wa ghala ambayo bado hayajakidhi vigezo vilivyowekwa, ili yaweze kuboreshwa na kutoa huduma bora, salama na zenye kuaminika kwa wakulima na wawekezaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema kuwa tukio la kufunga na kufungua msimu wa mauzo ya mazao limekuwa chachu na hamasa kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Ameongeza kuwa mfumo huo umeongeza uwazi, ushindani wa bei na kuongeza kipato cha wakulima, jambo linalochangia maendeleo ya kiuchumi ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Sambamba na hayo Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala  Bw.Asangye Bangu, ameeleza kuwa msimu wa 2025/2026 umeweka rekodi ya mauzo ya tani milioni 1.1 za mazao kupitia mfumo huo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na msimu uliopita. Amefafanua kuwa wakulima wamejipatia mapato ya Shilingi trilioni 2.4, huku mazao ya korosho, mbaazi na ufuta yakiongoza kwa kiasi cha mauzo.
Bangu ameongeza kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kupanuka kwa kasi, ambapo umeongezeka kutoka wilaya 65 hadi 114, idadi ya waweka mali imeongezeka kutoka 224 hadi 788, mapato ya Halmashauri yamefikia Shilingi bilioni 65, ajira zaidi ya 11,430 zimezalishwa, na idadi ya leseni za maghala imefikia 286. Mafanikio hayo, amesema, yanaonesha mchango mkubwa wa mfumo katika kukuza uchumi wa wakulima na kuimarisha mapato ya Serikali za Mitaa.

Katika mwelekeo wa msimu wa 2026/2027, WRRB imelenga kupanua wigo wa mfumo kwa kuingiza sekta za mifugo, ngozi na mwani, ili kutoa fursa zaidi za kiuchumi kwa wadau wa sekta hizo. Aidha, imehimiza sekta binafsi kuwekeza katika uanzishaji wa maghala bora, ikiwemo maghala yanayohamishika, ili kuongeza upatikanaji wa huduma za uhifadhi na biashara ya mazao katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa ujumla, hafla hiyo imeonesha dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kama nyenzo muhimu ya mageuzi ya kilimo na biashara ya mazao, kwa lengo la kumwinua mkulima, kuongeza ushindani wa masoko na kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi wa Taifa.