Waziri Mkuu Asema Asilimia 20 ya Mapato ya Mazao Ielekezwe Kwenye Ujenzi wa Maghala Karibu na Wakulima
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema asilimia 20 ya mapato yatokanayo na mazao ya kilimo inapaswa kuelekezwa katika ujenzi wa maghala karibu na maeneo ya uzalishaji ili kupunguza gharama kwa wakulima na kuongeza ufanisi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala nchini.
"Asilimia 20 ya mapato yanayotokana na mazao ya kilimo inapaswa kuelekezwa katika ujenzi wa ghala kwenye maeneo ya uzalishaji ili wakulima wasipate shida ya kusafirisha mazao yao umbali mrefu," amesema.
Waziri Mkuu amesema hayo leo Mei 19, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, yenye kaulimbiu isemayo "Mfumo Imara, Uchumi Endelevu."
Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu pia alizindua rasmi Mkakati wa Uhamasishaji wa Matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unaolenga kuongeza uelewa na ushiriki wa wakulima, wafanyabiashara, vyama vya ushirika, taasisi za fedha pamoja na wadau wengine katika matumizi ya mfumo huo nchini.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo huo kwa kuwa umechangia kuongeza uwazi na ushindani katika biashara ya mazao pamoja na kuhakikisha wakulima wananufaika na thamani halisi ya mazao yao.
"Pale ambapo kuna changamoto, mbadala wake si uholela. Mbadala wake ni kushughulikia changamoto zinazojitokeza," amesema.
Aidha, amesema changamoto ya umbali wa maghala haitatatuliwa kwa kurejesha mifumo isiyo rasmi ya biashara ya mazao bali kwa kujenga maghala karibu na maeneo ya uzalishaji.
"Jawabu la changamoto ya umbali wa maghala si kurejesha uholela. Jawabu ni kujenga maghala karibu na wananchi ili wakulima wasipate shida ya kusafirisha mazao yao umbali mrefu,"
