Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
UJUMBE WA TANZANIA WATEMBELEA CHEMBA YA WAFANYABIASHARA NCHINI UTURUKI
09 Sep, 2025
UJUMBE WA TANZANIA WATEMBELEA CHEMBA YA WAFANYABIASHARA NCHINI UTURUKI

UJUMBE WA TANZANIA WATEMBELEA CHEMBA YA WAFANYABIASHARA NCHINI UTURUKI
Istanbul, Septemba 8, 2025 – Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari, ulitembelea Chemba ya Wafanyabiashara ya Istanbul (Istanbul Chamber of Commerce) na kufanya mazungumzo na Ndg. Ahmet Özer, Makamu wa Rais wa Jumuiya hiyo. Taasisi kutoka Tanzania zilizoshiriki ziara hiyo ni Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara ili kuweka msukumo wenye tija na kuongeza wigo wa fursa za kimkakati. Vilevile, kujadili mwenendo wa biashara baina ya nchi hizi mbili hususan namna bora ya kuongeza kiwango cha biashara (volume of trade) kufikia Dola za Marekani Bilioni Moja (1 billion USD). Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi, aliwasilisha fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania kwenye sekta za madini, kilimo, ufugaji, utalii, na miundombinu na kukaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uturuki kuzitumia. 
Chemba ya Wafanyabiashara ya Uturuki ilisifu ushirikiano mzuri wa biashara uliopo na Tanzania.  Wakati wa mazungumzo hayo, Ndg. Özer na ujumbe wake waliarifu kwamba Uturuki imekuwa ikifanya biashara na nchi yetu hususan kununua mazao na matunda na ingependa kuona biashara kati ya nchi hizi mbili inakua zaidi. Hivyo, alibainisha utayari wa kushirikiana na Tanzania ili kuongeza kiwango hicho cha biashara kwa maslahi ya pande mbili. Aidha, alieleza dhamira ya chemba za Tanzania na Uturuki kushirikiana kwa karibu ili kukuza sekta ya biashara. Kabla ya kuhitimisha mazungumzo hayo, ujumbe wa Tanzania ulitoa mwaliko kwa wafanyabiashara kutoka Uturuki kwenda nchini Tanzania ili kukutana na wenzao kwa ajili ya majadiliano ya kina kuhusu ushirikiano kwenye sekta za kimkakati. 

Kufanyika kwa ziara hii ni ishara nzuri ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano baina ya mataifa haya katika sekta za uchumi. Tanzania imejidhatiti kutumia fursa za ushirikiano huo ili kuimarisha biashara ya sasa, kuongeza maeneo mapya, kuvutia zaidi wafanyabiashara kutoka Uturuki kuja Tanzania, sambamba na Watanzania kwenda Uturuki kuuza bidhaa za Tanzania kwenye soko la nchi hiyo.