Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
WAKULIMA kuanza kupata pensheni ya uzeeni
20 Jul, 2022
WAKULIMA kuanza kupata pensheni ya uzeeni

WAKULIMA wanaouza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wanatarajia kuanza kupata pensheni ya uzeeni.

Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu Akizungumza na vyama vya Ushirika vya Msingi vya Ligunga,Namatili na  Mtetesi katika Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma na wakulima wa Chama cha Msingi Nanyumbu mkoani Mtwara amesema,serikali imedhamiria kuhusisha Mfumo wa stakabadhi ghalani na pensheni kwa wakulima ili wakulima waweze kumudu kuendesha maisha yao wanapokuwa wazee.

Amesema uwezo wa kufanya kazi kwa wakulima  wakiwa vijana ni tofauti na wanapofikisha miaka 60 hivyo wakulima watakaokuwa wanauza kwenye Mfumo wa stakabadhi ghalani michango yao kidogo kidogo itafanyika  kwenye mfumo ili kujiwekea pensheni uzeeni.

"Nguvu zinapokuwa zimepungua,mashamba bado unayo hivyo pensheni itawawezesha wakulima wazee kuendelea kupata fedha za kuwalipa vibarua watakaokuwa wanawafanyia kazi za kilimo",alisisitiza Bangu.

Hata hivyo amesema pensheni hiyo kwa wakulima itaunganisha na mambo mengine muhimu kwa wazee kama Bima za Afya na mikopo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo,Serikali ipo katika hatua za awali za kuhakikisha kuwa suala la pensheni kwa wazee linafanikiwa.

Bangu amebainisha kuwa wataalam Kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakishirikiana na Bodi (WRRB) watapita kwa wakulima  ambao watapenda kujiunga kwenye mfumo huo ili kutoa elimu ya uelewa kabla ya kuanza utekelezaji wake.