Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA UMEONGEZA USHINDANI WA SOKO LA MAZAO - DKT SULEIMAN SERERA ,NAIBU KATIBU MKUU 
23 Oct, 2025
MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA UMEONGEZA USHINDANI WA SOKO LA MAZAO - DKT SULEIMAN SERERA ,NAIBU KATIBU MKUU 

MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA UMEONGEZA USHINDANI WA SOKO LA MAZAO - DKT SULEIMAN SERERA ,NAIBU KATIBU MKUU 
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, ametoa wito kwa wadau wa kilimo na biashara kuendelea kutumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani (Warehouse Receipt System) ambao umeleta ushindani katika soko la mazao ya kilimo na kuwawezesha wakulima kunufaika kwa kupata bei nzuri za mazao yao.

Dkt. Serera alitoa wito huo Oktoba 22, 2025, alipotembelea maghala ya Karatu Gilole, Rhotia na Union Service Store (NMC) mkoani Arusha, yanayotumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani, kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na kusikiliza changamoto zinazowakabili wadau wa mfumo huo.

Akipongeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Dkt. Serera alisema bodi hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa katika halmashauri ya Karatu, hatua ambayo imeleta tija kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao.

Aidha, alisema Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imejipanga kuhakikisha bidhaa zote zinazofika kwa mlaji zinakuwa salama na zenye ubora unaoendana na viwango vya usalama wa chakula, ili kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayotokana na matumizi ya vyakula visivyo salama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, alisema mfumo huo umepokelewa vyema na wakulima wa mazao mbalimbali ikiwemo mbaazi wilayani Karatu, na umechangia kupatikana kwa bei nzuri sokoni.

“Tunawahakikishia wanunuzi na watumiaji kwamba bidhaa zinazotolewa kupitia mfumo huu zina ubora unaoendana na thamani ya fedha zao. Mfumo huu unaleta uwazi, usawa na faida kwa pande zote,” alisema Bw. Bangu.

Naye Bi Gladness Tarimo, mkusanyaji mali, alisema mfumo wa Stakabadhi Ghalani umeleta manufaa makubwa kwa vijana kwani umewapa fursa ya kuuza bidhaa zao kwa bei shindani na inayojulikana wazi sokoni.

Kwa upande wake, Evarist Silayo, mfanyabiashara wa mazao ambaye kampuni yake inamiliki maghala katika maeneo matatu nchini ikiwemo Karatu, alisema mfumo huo umeondoa upunjaji na kuongeza uaminifu kati ya wakulima na wanunuzi.