Mafunzo ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, amehitimisha rasmi mafunzo ya wakurugenzi wa ghala awamu ya tatu kwa msimu wa mbaazi na dengu yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 15 Agosti 2025.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Bw. Bangu amewasisitiza washiriki kwenda kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu, huku wakilinda ubora wa mazao yanayouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.
“Mfumo huu sasa unatumia zaidi teknolojia ya TEHAMA ili kuhakikisha kila hatua inafanyika kwa umakini, uwazi na ufanisi,” alisema Bw. Bangu.
Aidha, aliongeza kuwa mfumo wa stakabadhi za ghala unazidi kuongeza ajira kwa Watanzania kutokana na kupanuka kwa wigo wa huduma zake. Pia, mchakato wa kuingiza sekta ya mifugo katika mfumo huo uko mbioni kukamilika, jambo litakaloongeza thamani na wigo wa huduma za stakabadhi za ghala nchini.