Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU WA ZAO LA KAKAO JIJINI MBEYA
06 Mar, 2026
BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU WA ZAO LA KAKAO JIJINI MBEYA

BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU WA ZAO LA KAKAO JIJINI MBEYA
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, leo tarehe 5 Machi 2026 ameshiriki kikao cha wadau wa zao la kakao kilichofanyika jijini Mbeya. Kikao hicho kimeandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na mwelekeo wa zao la kakao nchini.

Katika kikao hicho, wadau walijadili Mambo mbalimbali ikiwemo kilimo cha mkataba, mwongozo wa biashara ya kakao kwa msimu wa 2025/2026 kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala pamoja na matumizi ya minada ya kidijitali katika kuuza zao hilo.

Akitoa salamu za Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu ameipongeza COPRA kwa kuandaa kikao hicho muhimu kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa zao la kakao ili kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuendeleza na kuimarisha sekta ya kakao nchini.

Aidha, Bw. Bangu amewahakikishia wadau wa zao la kakao kuwa mfumo wa stakabadhi za ghala utaendelea kuwa nguzo muhimu katika uuzaji wa zao hilo. Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa kakao unapofikishwa katika ghala, kwani ubora huo humwezesha mkulima kupata bei nzuri sokoni. Ameongeza kuwa WRRB itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za mfumo huo, na yeyote atakayekiuka taratibu zilizowekwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, wadau wa kikao hicho wameeleza matumaini makubwa ya kuendelea kukuza uzalishaji wa zao la kakao nchini kwa kuongeza maeneo ya kilimo, ili kufikia lengo la serikali la kuzalisha tani 80,000 za kakao ifikapo mwaka 2030.

Pamoja na mafanikio yanayoonekana katika kilimo cha kakao, wadau pia wamebainisha changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa miche bora ya kakao, uhaba wa ghala ya kuhifadhi mazao, kukosekana kwa maeneo maalum ya kukausha kakao, uhaba wa viwanda vya kuchakata kakao pamoja na uwepo wa magonjwa yanayoathiri zao hilo.

Katika kuhitimisha kikao hicho, wadau walikubaliana juu ya maazimio kadhaa ikiwemo kuendelea kuimarisha ushirikiano miongoni mwa taasisi na wadau wa sekta ya kakao, kuhakikisha kakao yote inayofikishwa katika ghala au kupitia AMCOS inahakikiwa ubora wake kabla ya kupokelewa, kuendelea kuwajengea uwezo wataalam ili waweze kuwahudumia wakulima kwa ufanisi, kuweka utaratibu wa awali wa kufanya malipo kwa wakulima kupitia vyama vyao, pamoja na kuhakikisha taasisi zinakuwa na ofisi za kanda ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima na wadau wengine.