WRRB YAHITIMISHA SAFARI YA KIKAZI MKOANI MANYARA

MANYARA, 29 AGOSTI 2025
WRRB YAHITIMISHA SAFARI YA KIKAZI MKOANI MANYARA
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imehitimisha safari yake ya kikazi mkoani Manyara tarehe 29 Agosti 2025, ambapo timu ya Bodi imetoa taarifa ya ziara kwa Bi. Maryam Muhaji, Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, aliyepokea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo.
Katika ziara hiyo, timu ya WRRB ilitembelea wilaya za Simanjiro, Kiteto na Hanang’ kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala pamoja na kujadiliana na wadau juu ya maendeleo yake katika maeneo husika.
Kabla ya kuwasilisha taarifa hiyo kwa uongozi wa mkoa, WRRB ilifanya kikao kazi na Bodi ya Chama cha RIVACU, ambapo iliwasilishwa taarifa ya utekelezaji wa mfumo, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizojitokeza.
Kupitia majadiliano hayo, WRRB iliweza kutanzua changamoto zote za kiutendaji zilizobainishwa na pande hizo mbili na kukubaliana kuanzisha ukurasa mpya wa mashirikiano kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa stakabadhi za ghala, kuongeza ushirikiano na kuhakikisha manufaa zaidi kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, alisema:
"Tumejifunza mengi kutoka kwa wadau wetu wa Manyara. Tumeona mafanikio yaliyopatikana kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala lakini pia changamoto zilizojitokeza. Tumezielewa changamoto hizo na tayari tumekubaliana namna ya kuzitatua kwa kushirikiana na vyama vya ushirika na wadau wengine. WRRB itaendelea kusimamia mfumo huu kwa weledi na uwazi ili kuhakikisha wakulima wananufaika kwa kupata bei nzuri na huduma bora."
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, Bi. Maryam Muhaji, aliipongeza WRRB kwa ushirikiano na jitihada zake za kuwafikia wadau na kutanzua changamoto, hatua ambayo amesema inaleta utulivu na kuimarisha utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala mkoani humo.
Hata hivyo, Bi. Muhaji alieleza wasiwasi wa mkoa juu ya kushuka kwa bei ya mazao hususan mbaazi na dengu. Akijibu hoja hiyo, Bw. Bangu alisema:
"Mwenendo wa biashara ya mazao haya duniani kwa sasa unaonesha kushuka kwa bei. Hata hivyo, Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya India ili kunusuru mwenendo huo na kuwalinda wakulima wetu."
MWISHO.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB)