WRRB, COPRA na TMX Wafanya Kikao Kazi na RC Katavi Kuhakikisha Mahindi Yanauzwa Kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Msimu wa 2026
WRRB, COPRA na TMX Wafanya Kikao Kazi na RC Katavi Kuhakikisha Mahindi Yanauzwa Kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Msimu wa 2026
Mheshimiwa Mwamvua Mrindoko, Mkuu wa Mkoa wa Katavi leo tarehe 03 Januari 2026 amefanya kikao na Taasisi za Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Mamlaka ya Uthibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) wamefanya kikao kazi na Mh Mwamvua Mrikondo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, kwa lengo la kuhakikisha zao la mahindi linauzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Mwamvua Mrindoko amesema kuwa Mahindi ni moja ya mazao yanayozalishwa kwa wingi mkoani Katavi, hivyo kunahitajika mfumo madhubuti wa masoko ili kuwawezesha wakulima kupata bei yenye tija na kuongeza kipato chao. Alisisitiza kuwa mkoa uko tayari kuona Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ukiimarishwa na kupanuliwa ili kujumuisha mazao zaidi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa mkoa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema kuwa Bodi ipo tayari kuhakikisha maandalizi yote muhimu yanafanyika kwa wakati ili mahindi ya msimu wa 2026 yauzwe kupitia mfumo huo kwa ufanisi. Ameeleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi husika ni nguzo muhimu ya mafanikio ya mfumo huo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Mlola, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa kwa kushirikiana na ofisi yake pamoja na taasisi nyingine zinazohusika, ikiwemo WRRB na TMX, wataendelea kutatua changamoto zilizopo ili mfumo uweze kufanya kazi kwa ufanisi pindi msimu utakapoanza.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX Bw.Godfey Malekano ameeleza kuwa ili wakulima waweze kupata bei shindani sokoni, ni muhimu kuzingatia ubora wa mazao kuanzia hatua ya uzalishaji hadi uhifadhi. Amewasisitiza wataalamu wa kilimo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakulima juu ya umuhimu wa kuandaa mazao kwa viwango vinavyokubalika sokoni.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji), Afisa Kilimo wa Mkoa, Mrajis Msaidizi wa Mkoa, pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali wakiwemo Afisa Masoko kutoka WRRB, Mkurugenzi wa Ubora na Maendeleo ya Mazao kutoka COPRA, na Meneja wa COPRA Kanda ya Magharibi
