Mkurugenzi Mkuu WRRB Awahimiza Washiriki wa Mafunzo ya Ghala Kuongeza Ujuzi na Ufanisi wa Sekta
Leo, Machi 26, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) Bw. Asangye Bangu ametembelea na kuwasalimia washiriki wa mafunzo ya waendesha ghala yanayoendelea mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya juhudi za bodi hiyo kuimarisha ufanisi katika sekta ya uhifadhi wa mazao nchini.
Akizungumza na washiriki hao Bw. Bangu amewapongeza kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo muhimu hususan vijana kutoka mikoa mbalimbali walioweza kusafiri umbali mrefu kufika Morogoro kwa lengo la kuongeza maarifa na ujuzi wao Amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya vijana katika kujifunza na kuchangia maendeleo ya sekta ya Biashara na kilimo.
Aidha Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea washiriki uwezo wa kitaalamu katika uendeshaji na usimamizi bora wa ghala, ili kuhakikisha mazao yanahifadhiwa kwa viwango vinavyokubalika na kuongeza thamani ya mazao sokoni.
Bw. Bangu amesisitiza umuhimu wa washiriki kutumia elimu wanayoipata kwa vitendo ili kuboresha mifumo ya uhifadhi wa mazao kuongeza ufanisi wa biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.
Amehitimisha kwa kuwataka washiriki hao kuwa mabalozi wazuri wa elimu waliyoipata na kupeleka kwa wadau wengine ili kuongeza tija na uelewa mpana kuhusu umuhimu wa mfumo wa stakabadhi za ghala nchini.
