WRRB YATOA ELIMU YA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA KWA AMCOS SONGWE
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetoa elimu kuhusu Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS) kwa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ileje na Halmashauri ya Mji Tunduma, mkoani Songwe.
AMCOS zilizofikiwa ni Isongole, Bulambya, Nandanga na Migoneka, ambazo kwa pamoja zina zaidi ya wakulima 325 na zinanufaika na ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la Good Neighbors Tanzania.
Akizungumza Oktoba 1, 2026 katika mafunzo hayo ya siku tano yanayofanyika wilayani Ileje kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 3, 2026, Afisa Masoko Mwandamizi wa WRRB, Revocatus Mdumule, ameeleza namna wakulima wanavyoweza kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kuhifadhi mazao yao kwa kuzingatia ubora na kuyafikia masoko rasmi.
Mdumule amesema mfumo huo unatoa fursa kwa wakulima kukusanya mazao yao, kuyahifadhi katika maghala yenye leseni na kuyauza kupitia utaratibu rasmi wa soko, hatua inayosaidia kuongeza uwazi katika biashara ya mazao na kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Good Neighbors Tanzania yamewahusisha viongozi 30 kutoka AMCOS hizo, ambao wanatarajiwa kutumia elimu waliyoipata kuwafikishia wanachama wao uelewa kuhusu Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na fursa zinazopatikana kupitia mfumo huo.
