WRRB, TUME YA MADINI WATETA UUZAJI WA MADINI KUPITIA STAKABADHI ZA GHALA
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imekutana na Tume ya Madini kwa ajili ya kujadili mwongozo na uunganishaji wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), itakayowezesha madini kuuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS).
Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 2, 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Bw. Asangye Bangu amesema hatua hiyo inalenga kutanua wigo wa Mfumo wa Stakabadhi katika kuwezesha biashara nchini sambamba na kuongeza soko la madini kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.
“Kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika sekta ya madini, wachimbaji wadogo wataweza kupata uhakika wa masoko ya madini yao pamoja na kuwezeshwa kupata mkopo kutoka taasisi za kifedha kupitia na bidhaa iliyoingizwa ghalani" amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Biashara ya Madini Bi. Sundi Kilugala Malomo kutoka Tume ya Madini, amepongeza hatua ya WRRB katika kutanua wigo wa kuwezesha biashara kupitia mfumo na kuongeza kuwa kukamilika kwa mchakato huo kutaongeza tija kwa wachimbaji, wafanyabiashara na taifa kwa ujumla.
